For home theatre system solution

Saturday, February 18, 2012

DAR ES SALAAM

YANGA YALAZIMISHWA KUONGEA KIARABU NA ZAMALEK UWANJA WA TAIFA

Wachezaji wa timu ya Yanga wakishangilia mbele ya mashabiki wao mara baada ya mchezaji wa timu hiyo Khamis Kiiza, kuifungia timu hiyo goli la kuongoza katika kipindi cha kwanza,Tayari mpira umekwisha na timu ya Zamalek imefanikiwa kusawazisha goli na kufanya matokeo kuwa 1-1 mpaka mwisho wa mchezo.Huu ni mchezo wa mashindano ya Klabu bingwa barani Africa yanayoandaliwa na shirikisho la vyama vya mpira wa miguu (CAF), timu hizo zitarudiana tena nchini Misri baada ya wiki mbili zijazo.
Mmoja wa wachezaji wa Yanga akipiga mpira kuelekea lango la Zamalek huku mlinda mlango wa timu hiyo akijaribu kuzuia ili mpira huo usilete madhara katika lango lake.
Mashabiki wa timu ya Yanga wakiwa wamevamia kweny jukwaa la Simba ambalo mashabiki wa Simba wanakaa.
Wachezaji wa Yanga na Zamalek wakisalimiana kabla ya kuanza kwa mchezo huokwenye uwanja wa Taifa.
Marefarii wa mchezo huo wakiziongoza timu kuingia uwanjani tayari kwa kuanza kwa mchezo huo.
 
Chanzo: Kapingaz blog

Zimbabwe yaondolewa vikwazo na EU

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe

Muungano wa Ulaya umewaondolea vikwazo baadhi ya maafisa wakuu wa serikali ya Zimbabwe, ingawa utaendelea kushikilia mali ya rais wa nchi hiyo Robert Mugabe pamoja na washirika wake wa karibu.
Kwa mujibu wa muungano huo, vikwazo vya usafiri dhidi ya mawaziri wawili viliondolewa ili kushinikiza serikali kuharakisha mchakato wa mageuzi.

Lakini msemaji wa chama cha rais Robert Mugabe,alipinga hatua hiyo akitaja vikwazo hivyo kama vinavyokiuka sheria, vyenye misingi ya ubaguzi wa rangi na vitakavyoathiri uchumi wa nchi.
Muungano huo pia uliondoa takriban kampuni ishirini za serikali kwenye orodha hiyo ambazo muungano huo ulidai kuwa zilisaidia kufadhili vurugu nchini Zimbabwe.

Ingawa Zimbabwe imepiga hatua katika mchakato wa kuunda katiba mpya, na kuimarisha uchumi, Muungano huo ungali na wasiwasi ikiwa ahadi zilizowekwa baada ya uchaguzi uliokumbwa na vurugu mwaka 2008, ikiwemo ahadi za kufanyia mabadiliko idara ya polisi hazijaweza kutimizwa.

DAR ES SALAAM

Yanga, Zamalek hapatoshi leo. 

Na:Sosthenes Nyoni na Calvin Kiwia 
MABINGWA wa soka nchini, Yanga leo watashuka dimbani wakiwa na deni la kucheza kufa na kupona ili kuepuka kuithibitisha kauli ya wapinzani wao Zamalek ya Misri kwamba, wamekuja nchini kuwafanya wao kuwa ngazi ya kutwaa ubingwa wa Vilabu Afrika.
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Kocha Msaidizi wa timu ya Zamalek ya Misri Osama Nabil (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,katikati ni msemaji wa TFF Boniface Wambura anayefuata ni Kocha Mkuu wa Yanga Kostadin Papic pamoja na Nahodha wa Yanga Shadrack Nsajigwa.Picha na Mpiga picha Wetu.
 
Mchezo huo ulioteka hisia za mashabiki wa soka nchini, unatarajia kuwa mkali ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia majira ya saa 10 jioni.

Jana katika mkutano na waandishi wa habari jijini, Kocha Msaidizi wa Zamalek, Ossama Nabil alisema wamekuja Tanzania siyo tu kuifunga Yanga, bali nia yao kubwa ni kutwaa ubingwa baada ya muda mrefu.

Nabil alisema ni muda mrefu sasa umepita bila timu yao kutwaa taji kubwa la soka Afrika, hivyo fursa ya pambano la leo dhidi ya Yanga ambalo wana hakika watashinda ni njia nzuri kuelekea kurejesha taji hilo.

"Tunaiheshimu Yanga kama klabu kubwa na yenye uzoefu kwenye michuano hii, lakini pamoja na hilo kwa upande wetu tunataka kulirudisha kombe la michuano hii katika mikono yetu baada ya kulikosa kwa muda mrefu," alisema kocha huyo msaidizi.

"Tumekuja hapa siyo tu kuifunga Yanga, lakini pia mechi ya hiyo ni fursa yetu nzuri ya safari ya kutwaa taji tulilolikosa kwa muda mrefu sasa," alisema Nabil kwa kujiamnia.

Nabil alisema kuwa kikosi chake kiko imara na chenye kila utayari wa ushindani dhidi ya Yanga. "Tumekuja tukiwa tumejiandaa vizuri, tumekuja kufurahia ushindi."

Kwa upande wa Kocha, Kostadin Papic ambaye mwanzoni alionyesha kukata tamaa ya kuzaimisha Zamalek nyumbani, jana alitoa kauli za kujivunia maandalizi aliyofanya kwenye kikosi chake.
"Nimemaliza jukumu la maandalizi kwa timu yangu, nimendaa kikosi cha ushindani kinachojiandaa kukabiliana vizuri na Zamalek," alisema Papic katika mkutano na waandishi wa habari.

Papic hakutaka kuibeza Zamalek kama alivyofanya mwenzake, lakini yeye anaamini anacheza na moja ya timu bora kabisa katika soka la Afrika.

"Kama kocha nimemaliza kazi yangu, ninaweza kusema tupo tayari kupambana na Zamalek katika pambano hili gumu. Hatuna la zaidi uwanjani zaidi ya ushindi," alisema Papic

Pamoja na maandalizi hayo, Papic atashusha kikosi kitakachokuwa na makali pungufu kutokana na baadhi nyota wake kuwa nje kutokana na kuwa majeruhi.

Ni wazi kipa namba moja, Yaw Berko hatakuwa uwanjani leo, sawa kama ilivyo kwa viungo Salum Telela, Godfrey Bonny, Nurdin Bakar na Rashid Gumbo.

Na badala yake, Yanga itawategemea zaidi washambuliaji wake Devis Mwape na Kenneth Asamoa kupeleka mashambulizi langoni mwa Zamalek wakipitishiwa mipira na kiungo Haruna Niyonzima.

Kwa upande wa kikosi cha mafarao, mshambuliaji zamani wa Wigan Athetic, Amri Zaki ndiye anayetarajia kuwa mwiba mkali kwa Yanga sambamba na Mcameroon Alex Mdomo na Razack Thomas ambaye ni raia wa Benin.

Wakati huo huo, nyota wa zamani wa Yanga, Athuman Chama 'Jogoo' amemtaka kocha wa timu hiyo, Mserbia Kostadin Papic kutumia mfumo wa 4-4-2 badala ya 4-3-3 kwenye pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek.

Beki huyo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars alisema: "Tangu Papic alivyotua nchini mwaka jana kukinoa kikosi cha Yanga amekuwa akitumia mfumo wa 4-3-3," alisema Chama.
Amekuwa akiwachezesha Mwape, Asamoah na Kiiza nafasi ya ushambuliaji wakati Kijiko, Seme na Niyonzima wakicheza katikati ya kiwanja.

"Sioni kama mfumo huo unatoa matumaini chanya yakuishinda Zamalek kwa leo, ambao wana uwezo mkubwa wakumiliki mpira na kupiga pasi kutoka njuma hadi mbele kushambuliaji," alisema Chama.

Alisema anafikiri mfumo wa 4-4-2 ndio utatoa nafasi kubwa kwa Yanga kuweza kuwadhibiti vilivyo Waarabu hao.

"Unavyotumia mfumo wa 4-4-2 ina maana utakuwa na wachezaji wanne katikati ya kiwanja ambao watakuwa na kazi ya kuzuia na pia kushambulia kwa wakati mmoja," aliongeza Chama.
"Lakini unavyotumia 4-3-3 unapunguza mtu mmoja katikati ya uwanja na kumpeleka mbele kushambulia, zitaki kuamini kwamba Kiiza ana uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji," alisema.

Alishauri kocha huyo kutumia mfumo wa 4-4-2 kwa lengo la kuwadhitibiti Zamalek na kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye pambano hilo la awali na kujiweka katika mazingira mazuri kusonga mbele ya michuano hiyo. 

Chanzo: Mwananchi Communications Ltd