For home theatre system solution

Wednesday, February 22, 2012

Mwanafunzi adaiwa kuishi na mke

John Gagarini, Kibaha
SAKATA la wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mwanalugali, wilayani Kibaha limeibua mambo mapya baada ya kubaini kuwa mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo ameoa na anaishi na mke.

Hayo yamebainika siku chache baada ya shule hiyo
kuwasimamisha wanafunzi 30 waliokuwa wakiunda vikundi vya Al-Qaida na Al-Shabab huku mmoja akituhumiwa kumpiga mwalimu wake.

Hivi karibuni zilitokea vurugu kati ya makundi ya wanafunzi wa shule hiyo baada ya kutofautiana na kusababisha kuitishwa kwa mkutano wa wazazi na walimu.Pia imebainika kuwa wanafunzi wa kike ambao wako kwenye makundi hayo kuwa wakijihusiha na masuala ya mapenzi na vijana hao.

Taarifa zaidi zimebainisha kuwa wanafunzi ambao wako kwenye makundi hayo wamekuwa wakikiuka taratibu za shule na wanapoadhibiwa wamekuwa wakijiunga na makundi hayo.

Pia imebainika kuwa wanapokuwa kwenye vijiwe ambavyo viko jirani na shule hiyo wamekuwa wakivuta bangi.

Moja ya wazazi ambao walihudhuria mkutano wa wazazi na walimu wa shule hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema vitendo hivyo, vimekuwa vikifanywa na wanafunzi hao na kwamba mmoja ana mke na mtoto mmoja.

"Huyu tunamfahamu kuwa ana mke na mtoto, na siku moja alitumia panga kutaka kuwapiga wenafunzi wenzake akidai kuwa wamemchongea kuwa yuko kwenye moja ya makundi hayo, je ataweza kusoma kwa mtindo huo," alisema mzazi huyo.

Alisema wanamfahamu vizuri mwanafunzi huyo na kusema kuwa hali ya mwanafunzi kuwa na mke ni jambo ambalo halifai kufumbiwa macho kwani kwa kigezo hicho asingestahili kuwa shuleni.

Moja ya walimu wa shule hiyo ambaye naye hakutaka kutajwa jina lake alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikiuka taratibu za shule ikiwa ni pamoja na kuharibu suruali na kuzibana maarufu kama ‘modo’ kwa wale wa kiume na wale wa kike kuvaa sketi fupi ‘kimini’.

"Kuanzia sasa mwanafunzi wa kiume atakayekuja na suruali ya kubana tutaichana mguu mmoja na wa kike tutaichana, je wazazi mnakubalina na hilo, kama kuna mzazi hakubaliani na hili aseme kwani moja ya vitu vinavyoharibu wanafunzi ni mavazi, mwanafunzi wa kike kikianguka kitu
chini ukimwambia aokote ni aibu alisema mwalimu huyo," alisema mwalimu huyo.

Kwa pamoja wazazi na wa wawanafunzi hao walikubalina kuwa endapo mwanafunzi atakwenda na nguo ambayo iko kinyume na sare za shule, zitaharibiwa ili kurejesha nidhamu kwenye shule hiyo.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Aron Ndunguru alisema walimwita baba wa kijana anayedaiwa kuuoa, lakini baba yake alikanusha na kusema kuwa wanamsingizia mtoto wake.

Ndunguru alisema tangu kutokea kwa vurugu za wanafunzi wa vikundi hivyo, mwanafunzi huyo hajafika shuleni tangu mwaka jana na kwamba wanaendelea na uchunguzi.
 
Chanzo:www.networkedblog.blogspot.com

SERIKALI RUVUMA YAPIGA 'STOP' MAANDAMANO YA WAENDESHA PIKI PIKI WANAOPINGA MAUWAJI YA KISHIRIKINA

Serikali imesikitishwa na tukio la kundi la Vijana waendesha pikipiki maarufu kama yebo yebo kufanya maandamano katika Mitaa ya Manispaa ya Songea na kusababisha vurugu kubwa na uhalibifu wa mali.
Akitoa tamko hilo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ameeleza kuwa kwa muda wa siku tatu zilizopita kumekuwepo na tetesi za kutokea mauaji kwa imani za kishirikina zenye kulenga zaidi akinamama kuondoa sehemu za mwili kuwasaidia mambo ya kibiashara hivyo kupelekea watu kufariki.
Kufuatia matukio hayo mkoa uliagiza Jeshi la polisi kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo kwa kufanya uchunguzi wa wanaojihusisha na mauaji hayo kazi inayoendelea hadi sasa.
Katika maandamano ya leo watu wawili wamefariki dunia kwa kupigwa risasi wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji hao waliokuwa wakiwarushia mawe polisi wa kutuliza ghasia
Aidha Mkuu wa mkoa amewasihi wananchi wa Songea na Ruvuma kwa pamoja wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu ili vyombo vya ulinzi na Usalama viendelee kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha wote wanaojihusisha na biashara hii haramu wanachukuliwa hatua za kisheria
Ametoa wito wananchi kuwabaini watu wanaondesha uhalifu kwa njia ya uchawi na ushirikina na ambao wanaishi katika Mitaa yetu kwa kutoa taarifa zao kwa viongozi wa Mitaa na vyombo vya ulinzi na Usalama mapema.
“Serikali haimini kuhusu ushirikina wala uchawi.Inaelewa kuhusu tiba asilia na kwa tiba hizi hufanywa na watu wanaopewa vibali na serikali” alisema na kusisitiza kuwa wananchi wa Ruvuma wakatae ushirikina wa kiwango hicho pia uendeshaji wa ramli chonganishi zenye lengo la kugombanisha ndugu,jamii na Taifa kwani madhara yake ni kutokea mauaji kama haya kwa wasio na hatia.
Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi wa Ruvuma kutoa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na Usalama katika kipindi hiki kwa kuwabaini wote wanaojihusisha na kuendeleza uhalifu huu kwa vigezo vya uchawi na ushirikiana
Amewaagiza watendaji wa Mitaa,kata na Tarafa kuhakikisha ulinzi kwa kushirikiana na Polisi wanaendesha operesheni katika Mitaa yote na nyumba za kulala wageni ili kuwabaini wahalifu wote huku hatua za kisheria zikichua mkondo.
“Sote tukiungana hawa wachawi,waganga wa jadi na majambazi wanaodandia humo tunaweza kuwadhibiti ili mauaji yakome na Songea irudie utulivu wake kama kawaida” alisema Mkuu wa Mkoa
Kwa mujibu wa taarifa za polisi jumla ya watu watano hadi sasa wameripotiwa kuuwawa kwa hisia za ushirikina na uchawi katika maeneo ya Lizaboni, Bombambili na Matarawe kati yao wanawake watatu na wanaume wawili.Hata hivyo kati yao hakuna hata mmoja aliyeondolewa kiungo cha mwili kama wanavyodia baadhi ya wananchi waliondamana.
Imetolewa na
Revocatus A.Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa Ruvuma
22 Februari 2012

Chanzo: www.francisgodwin.blogspot.com

Polisi waua Songea






Kuna raia wanauawa tangu juzi na matukio yanaripotiwa ila askari hawachukui hatua yeyote ile zaidi wanasema ushahidi hawajauona,usiku wa kuamkia leo limekua tukia la 5 raia kuuliwa na askari kama kawaida yao hawatoi ulinzi kwa raia wao.

Asubuhi raia (Watoto, vijana, wazee) wakaamua kuwatolea uvivu askari na kuandamana hadi kituo cha polisi kudai haki ya kulindwa na kuishi raia walikua wengi kuliko uwezo wa askari wa kile kituo hivyo waliona hapa wakiwa wakali kituo kitachomwa moto maaana walikuja na jazba raia wakawaambia taarifa ziko kwa mkuu wa wilaya raia bila simile wakaanza maandamano hadi kwa mkuu wa wilaya kufika huko naye akanawa mikono kama pilato akasema mkuu wa mkoa ndo liko mikononi mwake.

Raia hawakuishia hapo wakalianzisha hadi kwa mkuu wa mkoa huku wakiimba "TUMECHOKA KUUWAWA" hadi kwa mkuu wa mkoa, hapo ndo movie ilpoanzia kumbe raia wakati wanaenda kwa mkuu wa mkoa inaaminika simu zilipigwa kwa mkuu wa mkoa na askari wanaolinda (FFU) wakafunga geti hapo ndo ikawa vuta nikuvute raia wakaweka kambi nje huku wanaimba nyimbo "MKUU WA MKOA UNAWAOGOPA RAIA WAKO JIUZURU", muda si mrefu gari ya FFU likawasiri likiwa na askari wa kutosha kwa vile raia hawakua na silaha wala ugomvi wakaamua kubaki huku wanaimba.

Askari kama kawaida yao wakawa wanazidi kusogelea huku wakitoa ishara wananchi watawanyike huku wananchi wakigoma hawatoki hadi mkuu wa mkoa naye atoke nje hapo ndo askari wakaanza kufyatua risasi za moto na raia wawili wakafa.habari zikafika mjini raia wameuliwa na askari hapo ndo mji ukazizima raia wakaingia mitaani askari waliokua mitaani walianza kupata upinzani mkali hadi askari wawili wamekufa hadi hivi sasa, imebidi jeshi liingilie kati na mji wote kufungwa hivi sasa mjini ni makundi ya wanajeshi na askari ndo yametawala hakuna maduka wala mabenki yanayofanya kazi
Chanzo: www.kingkif.blogspot.com

SONGEA

HALI SI SHWARI MJINI SONGEA LEO : POLISI WATUMIA SILAHA ZA MOTO KUTAWANYA MAANDAMANO YA WANANCHI SONGEA

Polisi wakiwa katika gari lao wakati wa kutuliza vurugu zinazoendelea wakati huu mjini songea baada ya wakazi wa manispaa hiyo kuandamana kupinga mauaji ya raia wasio na hatia yanayofanywa na watu wasiojulikana.
Polisi wakiwatawanya na kuwakamata baadhi ya waandamanaji hao katika manispaa ya Songea baada ya wakazi wa manispaa hiyo wengi wao wakiwa madereva wa pikipiki kuandamana hadi ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma kupinga mauaji ya watu yanayoendelea kwa kasi mjini humo ambao hadi sasa jeshi la polisi halijafanikiwa kuwakamata wauaji.
Madereva wa pikipiki wakiwa wamefunga barabara ya Songea kwenda Tunduru karibu na lango la kuingilia ofisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma,wakilitaka jeshi la polisi mkoa huo kuchukua hatua dhidi ya mauaji ya watu yanayoendelea mjini songea ambapo hadi sasa zaidi ya watu 8 wameuawa na watu wasiojulikana wengi wao wakiwa ni madereva wa pikpiki.

NA MUHIDIN AMRI,SONGEA

JESHI la polisi mkoani Ruvuma limelazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma na kituo kikuu cha polisi Songea mjini hali iliyopelekea shughuli mbalimbali kusimama.

Hali hiyo ilianza kujitokeza majira ya asubuhi ambapo wananchi wa mtaa wa Lizaboni wengi wakiwa ni madereva wa pikpiki walianza kujikusanya na kuanza maandamano kuelekea kituo kikuu cha polisi kilichopo karibu na uwanja wa majimaji mjini hapa.

Wananchi hao walikuwa wakiimba nyimbo za kulaumu jeshi la polisi wakidai kuwa limeshindwa kudhibiti mauaji yanayoendelea kujitokeza mjini hapa kila mara ambapo hadi sasa zaidi ya watu kumi wameshauawa na watu wasiojulikana.

“Tumeamua kuandamana kwani kimsingi mauaji yamezidi kutokea mjini hapa jana ameuwawa mtu,juzi na usiku wa kuamkia leo ameuwawa mwendesha pikipiki na abiria wake”walisikika wakisema.

Baada ya wananchi hao kukaribia kituo cha polisi walianza kurusha mawe na ndipo polisi walijihami kwa kutumia mabomu ya machozi ambapo wananchi hao na waendesha pikipiki walianza kukimbia ovyo na kupeleka maduka kufungwa kwa hofu ya kuibiwa.

Licha ya biashara mbalimbali kusimama pia ofisi za serikali ikiwemo ofisi ya mkuu wa mkoa na ya mkuu wa wilaya Songea zilifungwa kwa kuhofia waandamanaji kuingia kwenye ofisi hizo na kufanya uharibifu.

Kabla ya maandamano ya leo februari 20 mwaka huu wananchi kutoka kata ya Lizabon waliandamana hadi kwa mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Ole Sabaya kulalamikia kukithiri kwa mauaji katani humo ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wasiojulikana.

Akijibu malalamiko hayo mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa serikali itahakikisha ulinzi unaimarishwa na kwamba aliwataka kuimarisha ulinzi shirikishi ili kukabiliana na matukio hayo maovu.

Februari 19 mwaka huu mkazi wa Lizaboni Bakary Ally(20) aliuwawa kwa kukatwakatwa na mapanga na watu wasiojulikana ambapo februari 20 mwaka huu majira ya saa 3.00 usiku mtu mmoja mkazi wa mtaa wa Kipera shekhe Jamari(65) alikutwa ameuwawa kwa kukatwa mapanga kichwani na watu wasiojulikana wakati alipokuwa akielekea nyumbani kwake.

Marehemu Jamari alikuwa ni mmoja kati ya viongozi wa msikiti uliopo katika eneo hilo la Kipera.

Mauaji hayo yameendelea kujitokeza ambapo mwendesha pikipiki ambaye jina lake halikufahamika mara moja ameuwawa na watu wasiojulikana katika mtaa wa Mji Mwema mjini hapa usiku wa februari 22 mwaka huu na kupelekea wananchi mjini hapa kuishi kwa hofu kubwa.
 
Chanzo: www.latestnews.blogspot.com

SONGEA

BREAKING NEWS
VURUGU KUBWA ZAENDELEA KATI YA POLISI NA WANANCHI

Na Kalmas Konzo
Kwa habari zilizoufikia mtandao huu zinzsema kwamba kuna vurugu zinazoendelea kati ya polisi na wananchi mjini Songea.

Imasemekana kwamba polisi wanatumia mabomu na risasi katika kutuliza ghasia.

Pia inasemekana kwamba vurugu hizo zimesababishwa na maandamano ya raia wanaopinga mauaji ya ,ara kwa mara yanayotokea mjini Songea.

Habari kamili kuhusu tukio hili zitakujia hivi punde.


Copy right: www.tuburudike.blogspot.com