For home theatre system solution

Wednesday, February 29, 2012

DAR ES SALAAM

Mcheza filamu Marekani kuja nchini
Calvin Kiwia
MCHEZA filamu mahiri wa Marekani, Deidre Lorenz atashuhudia pambano la kimataifa lisilo na ubingwa kati ya Rashid “Snake Man” Matumla na bondia toka Russia 'The Rumble on the Mountain' utakaofanyika Moshi Juni 22, mwaka huu.

Akizungumzia ujio nyota huyo jana, Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Onesmo Ngowi alisema, Lorenz anayeishi New York, atawasili nchi hivi karibuni kwa ajili ya kushiriki kwenye mbio za Marie Frances Mt.Kilimanjaro Marathon kwa kumbukumbu ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.
Alisema mbio hizo zitafanyika kwenye mji wa Moshi Juni 24, mwaka huu zikianzia Moshi Club hadi Mamboleo madukani kupitia mzunguko wa YMCA.

Lorenz ambaye amecheza sinema nyingi ikiwemo sinema yake iliyompatia umaarufu mkubwa ya Santorini Blue iliyoiuzwa kwa zaidi ya dola za Kimarekani miloni 100, atapata pia fursa ya kushuhudia pambano hilo la masumbwi.

Alisema ujio wa mcheza sinema huyo unadhihirisha jinsi Tanzania hususani mlima Kilimanjaro unavyowavutia watalii wengi toka pande mbalimbali duniani.

Alisema pia, kutakuweko na mapambano ya utangulizi yatakayowashirikisha mabondia wa Tanzania, Kenya na Uganda. 

Pascal Bruno wa Tanzania atazichapa dhidi ya James Kitasi wa Kenya, Alibaba Ramadhani dhidi ya Sebyala Med wa Uganda, Allen Kamote dhidi ya Charles Damas, Simom Bernard dhidi ya Saidi Yazidu.

"Ujio wa Lorenz ni moja ya mikakati ya TPBC ikishirikiana na mashirikisho ya ngumi duniani kama IBF na CBC pamoja na majiji kadhaa hapa nchini kukuza ajira kwa vijana, kukuza utalii wa michezo (Sports Tourism) pamoja na kujenga mazingira mazuri kwa wawekezaji kuwekeza hapa Tanzania," alisisitiza Ngowi.

Baadhi ya sinema alizowahi kucheza Lorenz ni pamoja na: Santorini Blue, The Great Fight, The Emperor's Club, Le viager (2007), Focus Room (2003), Law & Order, Special Victims Unit, Baggage, August Rush, Perfect Stranger, BelzerVizion, Copy That, El Cantante na Two Weeks Notice.  

Chanzo: Mwananchi Communications Ltd

TAIFA STARS NGOMA DROO NA MSUMBIJI

 Ubao wa matangazo Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ukionesha matokeo yalivyo baada ya mechi ya Taifa Stars na Msumbiji ya kuwania kufuzu michuano ya Fainali za Mataifa Afrika, kumalizika leo jioni
 Mashabiki wa timu ya Taifa ya Msumbiji ambao asilimia kubwa walikodiwa nchini kuishangilia timu hiyo dhidi ya Taifa Stars, lakini ajabu baada ya Taifa Stars asilimia kubwa ya watu hao waliishangilia Stars
 Mpenda soka Ridhiwani Kikwete akiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela wakifurahi walipokutana katika mechi ya Taifa Stars na Msumbiji leo jioni, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Chanzo: richardmwaikenda.blogspot.com

Friday, February 24, 2012

SONGEA

Polisi wanne mbaroni kwa mauaji ya raia
Mtoto Shangwe Mtaula (16) mkazi wa Mabatini akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma alikolazwa baada ya kulipukiwa na bomu la machozi wakati wa vurugu zilizotokea mjini Songea.Picha na Joyce Joliga 
IGP MWEMA APELEKA KIKOSI CHA UCHUNGUZI, MAJERUHI HALI MBAYA  
Joyce Joliga na Kwirinus Mapunda, Songea  Polisi Mkoani Ruvuma, wanawashikilia na kuwahoji askari wake wanne kwa tuhuma za mauaji ya raia kwa kutumia risasi za moto katika vurugu zilizotokea juzi mjini Songea.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamhanda alisema jana kuwa askari hao walikamatwa na wanaendelea kuhojiwa ili kujua kama kulikuwa na uzembe katika utekelezaji wa majukumu yao.“Kwa kuwa tukio hilo limehusisha vifo, hatuwezi kuacha hivihivi tu ni lazima tujiridhishe kuwa askari hao hawakufyatua risasi kwa uzembe,”alisema Kamhanda.

 Kamanda huyo alisema askari hao watahojiwa baada ya kuundwa kwa tume maalumu ya kuchunguza tukio hilo, na tume hiyo ikibaini kuwa kulikuwa na uzembe, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo kamanda Kamhanda hakutaka kutaja majina, wala vyeo vya askari hao kwa maelezo kwamba ni ni mapema mno, pia sababu za kiusalama.Katika hatua nyingine Kamhanda alisema tayari watu 54 wamefikishwa mahakamani kutokana na vurugu za juzi.

IGP Mwema achunguza
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema ametuma kikosi cha maofisa waandamizi  kutoka  makao makuu ya jeshi hilo, kikiongozwa na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo, Kamishna Paul Chagonja kwenda mjini Songea kufanya uchunguzi wa ghasia hizo.

 Chagonja akizungumza na Mwananchi jana alisema maandamano  hayo hayakuwa ya amani bali ya kihuni kwani yalilenga kuvamia ofisi za serikali ikiwemo Ikulu ndogo na Ofisi ya Mkuu wa mkoa. Chagonja alikuwa akijibu swali lililotaka aeleze endapo haoni kama polisi imetumia nguvu kubwa kutawanya raia waliokuwa wakiandamana kwa amani.

"Maandamano ya amani watu wanavamia Ikulu, maandamano ya amani watu wanazingira ofisi ya mkuu wa mkoa?"
"Sijafika huko  ndo naelekea lakini, yale si maandamano ya amani. Yaani wahuni wanataka kuivuruga nchi waachiwe? Kuweni wazalendo, msiwe kama labda ninyi ni waandishi wa BBC kutoka Uingereza, hii ni nchi yenu."  

Alifafanua kwamba, maandamano ya amani yanafahamika kwani watu hulazimika kuomba kibali na kuweka wazi ajenda ya maandamano "Lakini siyo maandamano yale, watu hayakuwa na kibali chochote, wahuni wamejiingiza wanataka kuvuruga nchi tu."  

Mkuu huyo wa operesheni alitetea polisi akisema,"Usifikirie polisi hawana akili. Haiwezekani watu wazima na akili zao wenye mafunzo wafyatue hovyo risasi za moto kwa raia.  Hakuna askari anapenda kuua raia..., lakini watu wanavamia Ikulu, ofisi ya mkuu wa mkoa, magari ya polisi hapo kuna amani kweli?"

Alitoa angalizo kwamba ni lazima hata vyombo vya habari, viache ushabiki badala yake viangalie maslahi ya taifa kwani nchi ikivurugika wao pia hawatasalimika na kusisitiza, "Kuweni wazalendo bwana, msifikirie kulishutumu jeshi la polisi tu."  

Wakati IGP akituma kikosi hicho, wanaharakati, wanasiasa na wasomi wamekosoa matumizi makubwa ya nguvu za polisi dhidi ya raia na  waandamanaji waliokuwa wakifikisha ujumbe wao kwa mkuu wa mkoa kupinga mauaji ya watu tisa yaliyofanywa kwa imani za ushirikina.

Juzi wananchi waliokuwa wakiandama kupinga mauaji hayo, walipambana na polisi ambapo watu wanne waliuawa na wengine 41  kujeruhiwa.

Hali za majeruhi  Majeruhi wanane kati ya 11 waliolazwa katika Hospitali ya mkoa wa Ruvuma, jana waliruhusiwa. Majeruhi wengine 30 walipatiwa matibabu juzi na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao.

 Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedicto Ngaiza alisema tayari wagonjwa  wanane kati ya kumi na moja waliolazwa katika hospitali hiyo wameruhusiwa na kwamba ni wagonjwa watutu ndio waliobaki.
Mmoja wa wagonjwa hao, Shangwe Mtaula (16) mkazi wa Mabatini hadi jana alikuwa hajitambui kutokana na kipigo cha polisi kilichosababisha kuumia vibaya katika paji lake la uso.

Muuguzi wa wodi alimolazwa mgonjwa huyo, Hildetha Mhonyo  alisema binti huyo alifikishwa hospitalini hapo juzi saa tano asubuhi akiwa hajitambui na hivyo alilazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi.

Muuguzi huyo alisema, bado hali ya Shangwe si nzuri ingawa jana alianza kuzungumza kwa taabu na kwamba anaonekana kuwa na maumivu makali kwenye paji lake la uso, huku macho yake yaonekana kuvimba.Mgonjwa mwingine ni Esta Mbali (29)  mkazi wa Mshangano, ambaye amelazwa wodi namba tano baada ya kupigwa risasi katika bega lake la kushoto na kuumizwa vibaya.

Mgonjwa huyo anasema, hali yake inaendelea vizuri kwa sasa baada ya kupata matibabu.  Alisema, katu hatasahau tukio hilo kwani alikuwa akitoka hospiatali kumsalimia binamu yake ambaye alikuwa amejifungua na wakati akiwa njiani alikutana na kundi kubwa la watu wakiandamana na baadaye polisi walianza kuwatawanya kwa  mabomu ya machozi, ambapo  alifanikiwa kukimbia na kujificha kwenye nguzo ya umeme, lakini ghafla alisikia kitu cha moto kikimuumiza begani mwake .  Alisema alipatwa na kiwewe na kuanza kukimbia ovyo, hali iliyosababisha mwili mzima kulowa kwa damu ambayo wakati huo hakuweza kufahamu chanzo chake.

Esther aliendelea kusimulia kuwa baada ya kutokwa damu nyingi, aliishiwa nguvu na kuanguka, hadi aliposaidiwa na wasamaria wema ambao walimpakia kwenye gari na kumkimbiza hospitalini.
 Mwingine ni Sinje Mchompa  (29) mkazi wa Bombambili, ambaye alijeruhiwa  katika tukio hilo na kuumizwa vibaya na kipande cha  bomu  mdomoni eneo la SODECO, wakati alipokuwa akielekea Mabatini.

Sinje alisema alipokuwa katika eneo hilo ndipo vurugu zilianza na kwamba alishtukia akipigwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni kipande cha bomu mdomoni  na kutoboka  mdomo hali iliyosababisha meno kuuma sana.

Mgonjwa huyo ameomba msaada wa kupatiwa matibabu zaidi ili hali yake iweze kurejea kama awali.
 Kwa upande wake Matroni wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma Helta Soko, ametoa ushauri kwa wananchi kuacha tabia ya kufanya vurugu katika maeneo ya hospitalini kwani hali hiyo inasababisha usumbufu kwa wagonjwa waliolazwa.

Kauli ya Helta inatokana na baadhi ya wananchi kupiga kelele wakati walipokuwa wakiwarushia mawe wauguzi na askari waliokuwa wakipeleka mwili wa mmoja wa waliokufa katika tukio hilo  katika chumba  cha maiti. 

Habari tulizozipata wakati tukienda mitamboni zinasema, kwa mara nyingine, jana saa 12 jioni,  polisi mjini Songea walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwaokoa watu wawili waliokuwa wakipigwa na wananchi wakiwatuhumu kwamba ni majambazi wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya wananchi.

Watu hao ambao walijeruhiwa vibaya walikamatwa na wananchi katika eneo la Mkuzo nje kidogo ya Manispaa ya Songea baada ya kujitambulisha kwa wenyeji kwamba wao walikuwa wakitatafuta shamba la kununua, huku mmoja wao ambaye ni mwanamke akitoroka na kukimbilia kusikojulikana.

Kutokana na kuwatilia mashaka, wananchi hao waliwazingira na kuwaweka chini ya ulinzi kisha kuwafikisha nyumbani kwa kiongozi wa Serikali ya mtaa wa Mkuzo, John Moyo na baadaye walianza kuwapiga baada ya kutokea utata katika maelezo yao.

Kuona hivyo moyo alipiga simu polisi ambao walifika na kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi, hivyo kuwaokoa watuhumiwa hao kisha kuwakimbiza katika hosipitali ya mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya matibabu.

Watuhumiwa hao ambao wametambuliwa kwa majina ya Gervase na Juma, walikuwa wakivuja damu katika sehemu kadhaa za miili yao na polisi walipowafanyia upekuzi waliwakuta wakiwa na hirizi na nyaraka zilizoandikwa kwa lugha ambayo haikuwa rahisi kusomeka.

Chabzo: Mwananchi Communications Ltd

Thursday, February 23, 2012

Mauaji Songea
Askari wa kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Ruvuma wakiwa wamewakamata baadhi ya wananchi wakazi wa Lizabon ambao walikuwa wakifanya vurugu kwa kurusha mawe na kuchoma moto matairi barabarani jana wakati wa maandamano.Picha na Joyce Joliga 
POLISI WAUA RAIA WANNE WAJERUHI 41
Waandishi Wetu
MJI wa Songea na viunga vyake jana ulikumbwa na machafuko makubwa yaliyofanya polisi waue watu wanne baada ya wananchi kuandamana wakipinga mauaji yanayodaiwa kuambatana na imani za kishirikina tangu Novemba mwaka jana.

Katika machafuko hayo watu wengine 41 walijeruhiwa, wawili wakiwa katika hali mbaya huku shughuli za kiuchumi na kijamii zikisimama kwa muda.

Hata hivyo, idadi hiyo ya vifo na majeruhi inatofautiana kati ya ile iliyotolewa na jeshi la polisi, uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Wakati polisi ikisema waliokufa ni wawili na majeruhi ni 10, uongozi wa hospitali ya mkoa umesema umepokea maiti nne na majeruhi 41 na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inasema waliokufa ni wawili na majeruhi ni 20.

Tukio hilo la kwanza kutokea katika historia ya Mji wa Songea, lilitokana na hatua ya wananchi kuamua kuandamana kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuelezea kilio chao baada ya kuwepo kwa mauaji ya mara kwa mara ya raia tangu Novemba mwaka jana ambao baada ya kuuawa wamekuwa wakinyofolewa sehemu zao za siri.
Hadi jana, imeripotiwa kwamba watu tisa wameshapoteza maisha katika mazingira hayo kwa nyakati tofauti. Habari zilizopatikana mjini Songea zinasema kwamba mauaji hayo yanayohusishwa na imani za kishirikina yakidaiwa kufanywa na wachimba madini wa migodi iliyoko nchi jirani.
Maandamano na vurugu

Maandamano hayo yaliibuka baada ya jana asubuhi mtu mmoja wa kiume kukutwa amekufa kwa kukatwa mapanga eneo la Makarawe huku pia sehemu zake za siri zikiwa zimenyofolewa.

Baada ya kuuona mwili huo wa marehemu, umati wa watu ulianza kukusanyika na kuamua kuandamana wakisema kwa amani ili kuwasilisha kilio chao kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Maandamano hayo yalivuta umati watu na mamia ya wananchi walijiunga na kuanza kutembea kwa miguu huku wengine wakiwa katika pikipiki maarufu kwa jina la 'Yeboyebo,' kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa zilizo jirani na Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Ruvuma.

Kadri wananchi hao walivyokuwa wakiendelea kuandamana, habari zilitapakaa mitaa mbalimbali na kuwafanya wananchi wengi zaidi kuungana nao, hali iliyowalazimu polisi nao kujipanga kuwazuia kwa kutumia mabomu ya mchozi.

Hata hivyo, wananchi walizidi kuongezeka wakipinga hatua hiyo ya polisi kuwazuia kufikisha ujumbe wao kwa Mkuu wa Mkoa. Katika hatua hiyo, ndipo vurugu zilipoanza kwani wakati polisi watumia mabomu ya kutoa machozi, baadhi ya waandamanaji walianza kuvurumisha mawe hali iliyowafanya watu kukimbia huku na huko.

Vurugu zilishika kasi hali iliyowafanya polisi kuanza kutumia risasi za moto katika kile ilichodai baadaye kwamba ni katika kujilinda na ndipo vifo hivyo vilipotokea na idadi hiyo kubwa ya majeruhi. Hata hivyo, haikuelezwa mara moja kama miongoni mwa majeruhi hao alikuwamo askari polisi.

Baada ya mauaji hayo, vurugu zilizidi kusambaa katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Songea huku wananchi wakianza kurusha mawe kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi. Lakini wengine waliendelea kupigia kelele madai yao ya msingi huku wakilishutumu jeshi hilo kwa kushindwa kudhibiti mauaji hayo kwa muda mrefu.
Vurugu hizo zilisababisha ofisi za Serikali na taasisi binafsi mkoani Ruvuma kufungwa kwa muda yakiwemo maduka, masoko na huduma za kifedha katika mabenki kusimama kwa muda.

Huduma za usafiri katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani nazo zilisimama, huku madereva wa mabasi na abiria wakikimbia kujificha kuepuka mabomu ya machozi na risasi za moto zilizokuwa zikipigwa hewani.

Pia huduma za matibabu katika Hospitali ya Mkoa zilisimama kwa muda baada ya walinzi wa hospitali hiyo kufunga lango kuu, kutokana na wananchi wengi kukimbilia huko wakikimbia mabomu.

Habari zaidi kutoka eneo la tukio zimeeleza kuwa maandamano hayo yalichochewa na taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa juzi kwamba mauaji hayo yanahusiana na masuala ya kipenzi. Ilielezwa kwamba wananchi walikuja juu wakipinga madai hayo ambayo pia yaliripotiwa jana na gazeti hili.

Utetezi wa Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamhanda alisema polisi ililazimika kutumia nguvu ya ziada baada ya wananchi kukaidi amri ya kuwataka watawanyike.
Alidai waliopoteza maisha kutokana na vurugu hizo ni wawili na majeruhi 10 akisema watu hao walifariki dunia kwa kupigwa risasi za moto baada ya kukaidi amri ya polisi kutawanyika.

“Tulilazimika kutumia risasi za moto baada ya hawa vijana kukataa kutii amri ya polisi,” alisisitiza Kamanda Kamhanda.
Kamanda Kamhanda alisema watu 56 wamekamatwa kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na tukio hilo.
Kamanda Kamhanda alisema ingawa bado uchunguzi unaendelea, taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo cha vurugu hizo ni imani za kishirikina na siasa. Hata hivyo, hakufafanua ushirikina wala siasa zilivyochochea maandamano hayo.
RC atoa amri ya kutombea usiku

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema vurugu hizo zilizodumu kwa saa sita zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali na kuhatarisha usalama katika mji huo.

Kutokana na hali hiyo, alitoa amri ya kutotembea usiku akisema msako wa kuwasaka watuhumiwa wa maandamano hayo bado unaendelea.

“Kama watakuwa hawana shughuli za muhimu wabakie tu majumbani mwao ili kuepuka usumbufu. Polisi itaendelea kuwasaka watuhumiwa usiku ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa kauli hiyo baada ya kuongoza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kilichoitishwa ghafla kutokana na machafuko hayo makubwa.

Hospitalini
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedicto Ngaiza alisema kati ya watu nne waliokufa na miili yao kupokewa, miwili ilikuwa na majeraha ya risasi na majeruhi wawili  kati ya hao 41, walipelekwa chumba cha upasuaji kwa kuwa walikuwa na majeraha ya risasi pia.
“Hii miili ilikuja kwa awamu, mara ya kwanza ulikuja mmoja na mara ya pili ikaja mitatu. Yote ililetwa kwa magari ya polisi,” alisema Dk Ngaiza na kuongeza:
“Katika hii mitatu iliyokuja kwa pamoja miwili ilikuwa na majeraha ya risasi na mmoja alikuwa ni kijana aliyegonga mti na pikipiki akikimbia vurugu hizo. Kati ya majeruhi hao wawili wamepelekwa chumba cha upasuaji shida yao pia ni majeraha ya risasi.”

Kisa cha maandamano
Tangu Novemba mwaka jana, kumekuwa na matukio ya mauaji katika Mji wa Songea kwa nyakati tofauti hadi sasa ambayo yamekuwa yakitokea katika mazingira ya kutatanisha huku miili ya marehemu ikiwa imejeruhiwa kwa kukatwa mapanga, shoka au marungu na kunyofolewa sehemu za siri.

Hali imekuwa mbaya zaidi mwishoni mwa wiki ambako kwa siku tatu mfululizo mauaji hayo yalitokea hali iliyochochea hasira za wananchi hadi kufikia uamuzi wa kuandamana.

Watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo wanashikiliwa na polisi. Watuhumiwa ni Johari Kassim (16), Onesmo Hinju (14), Samason Haule (22) na Mussa Fuala (20) wote wakazi wa Mtaa wa Lizaboni mjini Songea.

Kilio chasikika

Kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imewataka watendaji na wenyeviti wa mitaa na mabalozi kuanzisha ulinzi wa doria za usiku katika maeneo yao kuanzia sasa na kwamba ambaye tukio la mauaji hayo ya kishirikina yatatokea katika mtaa wake atakamatwa na kuchukuliwa hatua.

Katika kikao cha kamati hiyo kilichowashirikisha pia viongozi hao, imeamuliwa pia kwamba watendaji hao wa ngazi ya msingi ya Serikali za Mtaa watalazimika pia kuwatambua wageni wote watakaofika katika maeneo yao ni pamoja na kuwataka waonyeshe vitambulisho vyao na wale watakaokuwa na shaka nao watoe taarifa zao katika vyombo vya sheria.

Habari hii imeandaliwa na Joyce Joliga, Kwirinus Mapumba Songea na Fredy Azzah, Dar

MBEYA

MVUA INAYOENDELEA KUNYESHA HIVI SASA JIJINI MBEYA YAHARIBU MIUNDOMBINU YA SOKO DOGO LA MWAMBENE

Hii ndio hali halisi ya soko la mwambene jijini mbeya mvua bado inaendelea kunyesha


Nyumba za jirani na soko hilo la mwambene zikiwa zimezungukwa na maji ya mvua inayoendelea kunyesha

Maji ya mvua yana pita katikati ya barabara ya kuelekea sokoni hapo


Mifereji ya kupitisha maji hayo ya mvua hakuna kabisa

Wednesday, February 22, 2012

Mwanafunzi adaiwa kuishi na mke

John Gagarini, Kibaha
SAKATA la wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mwanalugali, wilayani Kibaha limeibua mambo mapya baada ya kubaini kuwa mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo ameoa na anaishi na mke.

Hayo yamebainika siku chache baada ya shule hiyo
kuwasimamisha wanafunzi 30 waliokuwa wakiunda vikundi vya Al-Qaida na Al-Shabab huku mmoja akituhumiwa kumpiga mwalimu wake.

Hivi karibuni zilitokea vurugu kati ya makundi ya wanafunzi wa shule hiyo baada ya kutofautiana na kusababisha kuitishwa kwa mkutano wa wazazi na walimu.Pia imebainika kuwa wanafunzi wa kike ambao wako kwenye makundi hayo kuwa wakijihusiha na masuala ya mapenzi na vijana hao.

Taarifa zaidi zimebainisha kuwa wanafunzi ambao wako kwenye makundi hayo wamekuwa wakikiuka taratibu za shule na wanapoadhibiwa wamekuwa wakijiunga na makundi hayo.

Pia imebainika kuwa wanapokuwa kwenye vijiwe ambavyo viko jirani na shule hiyo wamekuwa wakivuta bangi.

Moja ya wazazi ambao walihudhuria mkutano wa wazazi na walimu wa shule hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema vitendo hivyo, vimekuwa vikifanywa na wanafunzi hao na kwamba mmoja ana mke na mtoto mmoja.

"Huyu tunamfahamu kuwa ana mke na mtoto, na siku moja alitumia panga kutaka kuwapiga wenafunzi wenzake akidai kuwa wamemchongea kuwa yuko kwenye moja ya makundi hayo, je ataweza kusoma kwa mtindo huo," alisema mzazi huyo.

Alisema wanamfahamu vizuri mwanafunzi huyo na kusema kuwa hali ya mwanafunzi kuwa na mke ni jambo ambalo halifai kufumbiwa macho kwani kwa kigezo hicho asingestahili kuwa shuleni.

Moja ya walimu wa shule hiyo ambaye naye hakutaka kutajwa jina lake alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikiuka taratibu za shule ikiwa ni pamoja na kuharibu suruali na kuzibana maarufu kama ‘modo’ kwa wale wa kiume na wale wa kike kuvaa sketi fupi ‘kimini’.

"Kuanzia sasa mwanafunzi wa kiume atakayekuja na suruali ya kubana tutaichana mguu mmoja na wa kike tutaichana, je wazazi mnakubalina na hilo, kama kuna mzazi hakubaliani na hili aseme kwani moja ya vitu vinavyoharibu wanafunzi ni mavazi, mwanafunzi wa kike kikianguka kitu
chini ukimwambia aokote ni aibu alisema mwalimu huyo," alisema mwalimu huyo.

Kwa pamoja wazazi na wa wawanafunzi hao walikubalina kuwa endapo mwanafunzi atakwenda na nguo ambayo iko kinyume na sare za shule, zitaharibiwa ili kurejesha nidhamu kwenye shule hiyo.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Aron Ndunguru alisema walimwita baba wa kijana anayedaiwa kuuoa, lakini baba yake alikanusha na kusema kuwa wanamsingizia mtoto wake.

Ndunguru alisema tangu kutokea kwa vurugu za wanafunzi wa vikundi hivyo, mwanafunzi huyo hajafika shuleni tangu mwaka jana na kwamba wanaendelea na uchunguzi.
 
Chanzo:www.networkedblog.blogspot.com

SERIKALI RUVUMA YAPIGA 'STOP' MAANDAMANO YA WAENDESHA PIKI PIKI WANAOPINGA MAUWAJI YA KISHIRIKINA

Serikali imesikitishwa na tukio la kundi la Vijana waendesha pikipiki maarufu kama yebo yebo kufanya maandamano katika Mitaa ya Manispaa ya Songea na kusababisha vurugu kubwa na uhalibifu wa mali.
Akitoa tamko hilo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ameeleza kuwa kwa muda wa siku tatu zilizopita kumekuwepo na tetesi za kutokea mauaji kwa imani za kishirikina zenye kulenga zaidi akinamama kuondoa sehemu za mwili kuwasaidia mambo ya kibiashara hivyo kupelekea watu kufariki.
Kufuatia matukio hayo mkoa uliagiza Jeshi la polisi kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo kwa kufanya uchunguzi wa wanaojihusisha na mauaji hayo kazi inayoendelea hadi sasa.
Katika maandamano ya leo watu wawili wamefariki dunia kwa kupigwa risasi wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji hao waliokuwa wakiwarushia mawe polisi wa kutuliza ghasia
Aidha Mkuu wa mkoa amewasihi wananchi wa Songea na Ruvuma kwa pamoja wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu ili vyombo vya ulinzi na Usalama viendelee kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha wote wanaojihusisha na biashara hii haramu wanachukuliwa hatua za kisheria
Ametoa wito wananchi kuwabaini watu wanaondesha uhalifu kwa njia ya uchawi na ushirikina na ambao wanaishi katika Mitaa yetu kwa kutoa taarifa zao kwa viongozi wa Mitaa na vyombo vya ulinzi na Usalama mapema.
“Serikali haimini kuhusu ushirikina wala uchawi.Inaelewa kuhusu tiba asilia na kwa tiba hizi hufanywa na watu wanaopewa vibali na serikali” alisema na kusisitiza kuwa wananchi wa Ruvuma wakatae ushirikina wa kiwango hicho pia uendeshaji wa ramli chonganishi zenye lengo la kugombanisha ndugu,jamii na Taifa kwani madhara yake ni kutokea mauaji kama haya kwa wasio na hatia.
Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi wa Ruvuma kutoa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na Usalama katika kipindi hiki kwa kuwabaini wote wanaojihusisha na kuendeleza uhalifu huu kwa vigezo vya uchawi na ushirikiana
Amewaagiza watendaji wa Mitaa,kata na Tarafa kuhakikisha ulinzi kwa kushirikiana na Polisi wanaendesha operesheni katika Mitaa yote na nyumba za kulala wageni ili kuwabaini wahalifu wote huku hatua za kisheria zikichua mkondo.
“Sote tukiungana hawa wachawi,waganga wa jadi na majambazi wanaodandia humo tunaweza kuwadhibiti ili mauaji yakome na Songea irudie utulivu wake kama kawaida” alisema Mkuu wa Mkoa
Kwa mujibu wa taarifa za polisi jumla ya watu watano hadi sasa wameripotiwa kuuwawa kwa hisia za ushirikina na uchawi katika maeneo ya Lizaboni, Bombambili na Matarawe kati yao wanawake watatu na wanaume wawili.Hata hivyo kati yao hakuna hata mmoja aliyeondolewa kiungo cha mwili kama wanavyodia baadhi ya wananchi waliondamana.
Imetolewa na
Revocatus A.Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa Ruvuma
22 Februari 2012

Chanzo: www.francisgodwin.blogspot.com

Polisi waua Songea






Kuna raia wanauawa tangu juzi na matukio yanaripotiwa ila askari hawachukui hatua yeyote ile zaidi wanasema ushahidi hawajauona,usiku wa kuamkia leo limekua tukia la 5 raia kuuliwa na askari kama kawaida yao hawatoi ulinzi kwa raia wao.

Asubuhi raia (Watoto, vijana, wazee) wakaamua kuwatolea uvivu askari na kuandamana hadi kituo cha polisi kudai haki ya kulindwa na kuishi raia walikua wengi kuliko uwezo wa askari wa kile kituo hivyo waliona hapa wakiwa wakali kituo kitachomwa moto maaana walikuja na jazba raia wakawaambia taarifa ziko kwa mkuu wa wilaya raia bila simile wakaanza maandamano hadi kwa mkuu wa wilaya kufika huko naye akanawa mikono kama pilato akasema mkuu wa mkoa ndo liko mikononi mwake.

Raia hawakuishia hapo wakalianzisha hadi kwa mkuu wa mkoa huku wakiimba "TUMECHOKA KUUWAWA" hadi kwa mkuu wa mkoa, hapo ndo movie ilpoanzia kumbe raia wakati wanaenda kwa mkuu wa mkoa inaaminika simu zilipigwa kwa mkuu wa mkoa na askari wanaolinda (FFU) wakafunga geti hapo ndo ikawa vuta nikuvute raia wakaweka kambi nje huku wanaimba nyimbo "MKUU WA MKOA UNAWAOGOPA RAIA WAKO JIUZURU", muda si mrefu gari ya FFU likawasiri likiwa na askari wa kutosha kwa vile raia hawakua na silaha wala ugomvi wakaamua kubaki huku wanaimba.

Askari kama kawaida yao wakawa wanazidi kusogelea huku wakitoa ishara wananchi watawanyike huku wananchi wakigoma hawatoki hadi mkuu wa mkoa naye atoke nje hapo ndo askari wakaanza kufyatua risasi za moto na raia wawili wakafa.habari zikafika mjini raia wameuliwa na askari hapo ndo mji ukazizima raia wakaingia mitaani askari waliokua mitaani walianza kupata upinzani mkali hadi askari wawili wamekufa hadi hivi sasa, imebidi jeshi liingilie kati na mji wote kufungwa hivi sasa mjini ni makundi ya wanajeshi na askari ndo yametawala hakuna maduka wala mabenki yanayofanya kazi
Chanzo: www.kingkif.blogspot.com

SONGEA

HALI SI SHWARI MJINI SONGEA LEO : POLISI WATUMIA SILAHA ZA MOTO KUTAWANYA MAANDAMANO YA WANANCHI SONGEA

Polisi wakiwa katika gari lao wakati wa kutuliza vurugu zinazoendelea wakati huu mjini songea baada ya wakazi wa manispaa hiyo kuandamana kupinga mauaji ya raia wasio na hatia yanayofanywa na watu wasiojulikana.
Polisi wakiwatawanya na kuwakamata baadhi ya waandamanaji hao katika manispaa ya Songea baada ya wakazi wa manispaa hiyo wengi wao wakiwa madereva wa pikipiki kuandamana hadi ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma kupinga mauaji ya watu yanayoendelea kwa kasi mjini humo ambao hadi sasa jeshi la polisi halijafanikiwa kuwakamata wauaji.
Madereva wa pikipiki wakiwa wamefunga barabara ya Songea kwenda Tunduru karibu na lango la kuingilia ofisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma,wakilitaka jeshi la polisi mkoa huo kuchukua hatua dhidi ya mauaji ya watu yanayoendelea mjini songea ambapo hadi sasa zaidi ya watu 8 wameuawa na watu wasiojulikana wengi wao wakiwa ni madereva wa pikpiki.

NA MUHIDIN AMRI,SONGEA

JESHI la polisi mkoani Ruvuma limelazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma na kituo kikuu cha polisi Songea mjini hali iliyopelekea shughuli mbalimbali kusimama.

Hali hiyo ilianza kujitokeza majira ya asubuhi ambapo wananchi wa mtaa wa Lizaboni wengi wakiwa ni madereva wa pikpiki walianza kujikusanya na kuanza maandamano kuelekea kituo kikuu cha polisi kilichopo karibu na uwanja wa majimaji mjini hapa.

Wananchi hao walikuwa wakiimba nyimbo za kulaumu jeshi la polisi wakidai kuwa limeshindwa kudhibiti mauaji yanayoendelea kujitokeza mjini hapa kila mara ambapo hadi sasa zaidi ya watu kumi wameshauawa na watu wasiojulikana.

“Tumeamua kuandamana kwani kimsingi mauaji yamezidi kutokea mjini hapa jana ameuwawa mtu,juzi na usiku wa kuamkia leo ameuwawa mwendesha pikipiki na abiria wake”walisikika wakisema.

Baada ya wananchi hao kukaribia kituo cha polisi walianza kurusha mawe na ndipo polisi walijihami kwa kutumia mabomu ya machozi ambapo wananchi hao na waendesha pikipiki walianza kukimbia ovyo na kupeleka maduka kufungwa kwa hofu ya kuibiwa.

Licha ya biashara mbalimbali kusimama pia ofisi za serikali ikiwemo ofisi ya mkuu wa mkoa na ya mkuu wa wilaya Songea zilifungwa kwa kuhofia waandamanaji kuingia kwenye ofisi hizo na kufanya uharibifu.

Kabla ya maandamano ya leo februari 20 mwaka huu wananchi kutoka kata ya Lizabon waliandamana hadi kwa mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Ole Sabaya kulalamikia kukithiri kwa mauaji katani humo ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wasiojulikana.

Akijibu malalamiko hayo mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa serikali itahakikisha ulinzi unaimarishwa na kwamba aliwataka kuimarisha ulinzi shirikishi ili kukabiliana na matukio hayo maovu.

Februari 19 mwaka huu mkazi wa Lizaboni Bakary Ally(20) aliuwawa kwa kukatwakatwa na mapanga na watu wasiojulikana ambapo februari 20 mwaka huu majira ya saa 3.00 usiku mtu mmoja mkazi wa mtaa wa Kipera shekhe Jamari(65) alikutwa ameuwawa kwa kukatwa mapanga kichwani na watu wasiojulikana wakati alipokuwa akielekea nyumbani kwake.

Marehemu Jamari alikuwa ni mmoja kati ya viongozi wa msikiti uliopo katika eneo hilo la Kipera.

Mauaji hayo yameendelea kujitokeza ambapo mwendesha pikipiki ambaye jina lake halikufahamika mara moja ameuwawa na watu wasiojulikana katika mtaa wa Mji Mwema mjini hapa usiku wa februari 22 mwaka huu na kupelekea wananchi mjini hapa kuishi kwa hofu kubwa.
 
Chanzo: www.latestnews.blogspot.com

SONGEA

BREAKING NEWS
VURUGU KUBWA ZAENDELEA KATI YA POLISI NA WANANCHI

Na Kalmas Konzo
Kwa habari zilizoufikia mtandao huu zinzsema kwamba kuna vurugu zinazoendelea kati ya polisi na wananchi mjini Songea.

Imasemekana kwamba polisi wanatumia mabomu na risasi katika kutuliza ghasia.

Pia inasemekana kwamba vurugu hizo zimesababishwa na maandamano ya raia wanaopinga mauaji ya ,ara kwa mara yanayotokea mjini Songea.

Habari kamili kuhusu tukio hili zitakujia hivi punde.


Copy right: www.tuburudike.blogspot.com

Tuesday, February 21, 2012

BREAKING NEWS

SUGU NA RUGE MUTAHABA WAPATANA



Hatimaye ugomvi wa Ruge Mutahaba na Mbunge wa jimbo la Mbeya kwa tiketi ya CHADEMA Mh. Joseph Mbilinyi (Sugu) umekwisha baada ya kufanyika kwa vikao mbali mbali chini ya Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, John Nchimbi na Mbunge Tundu Lisu.

Chanzo: www.djfetty.blogspot.com

NIGERIA

Jeshi la Polisi Nigeria lawauwa Boko Haram
 
 
Walinda usalama katika mji wa Maiduguri

Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kwamba wanajeshi watatu walijeruhiwa katika
makabiliano hayo ya risasi na kundi la Boko Haram.

Hata hivyo alikanusha kuwa kuna raia yeyote aliyeuwawa katika kisa hicho.

Lakini wenye maduka katika soko la Baga wamenukuliwa wakisema kuwa wameona maiti zipatazo ishirini hivi zikipakiwa kwenye lori.

Eneo hilo la Maiduguri ni ngombe kuu ya wapiganiaji wa Boko Haram . Na katika miaka ya hivi karibuni sehemu imeshuhudia milipuko kadhaa na ufyatuliananji wa risasi.

Tayari serikali ya rais Goodluck Jonathan imetangaza hali ya hatari katika mji huyo na miji menginea ambayo imeshuhudia mashambulizi toka kwa kundi hilo la Boko Haram.

Lakini wakazi wa miji hiyo wanasema kuwa suluhu ya kijeshi haijafaulu leta mafanikio yeyote

Chanzo: Global Publishers

NJOMBE

ANNA MAKINDA AWAASA WANANCHI WA NJOMBE

Na Kalmas Konzo
Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mbunge wa jimbo la Njombe kusini Mheshimiwa Anna Makinda amewataka wakazi wa Njombe kuwa wafanye kazi kwa bidii kuweza kuyafikia mafanikio katika maisha yao.

Mheshimiwa Anna Makinda ameyasema hayo pindi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Idundilanga katika kata ya Njombe mjini.

Anna Makinda amewataka wananchi waache kupiga soga vijiweni pasipo kufanya kazi kwani mafanikio hayawezi kuletwa na uvivu wa kutokufanya kazi.

Amewataka wananchi kuzitumia fursa zinazopatikana kama mradi wa Mchuchuma na Liganga katika kufanya kazi kwa bidii kwani fursa hizi huwa hzijitokezi mara mbili. Amewaasa kuwa fursa kama hizo zitaweza kuwaletea mafanikio wao wenyewe na mkoa wa Njombe kwa ujumla.

Copy right: www.tuburudike.blogspot.com

Monday, February 20, 2012

MAREKANI

DMX AVAMIWA APIGWA NONDO KICHWANI

Kijana mtanashati mjini Iringa maarufu kwa jina la DMX amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na vijana ambao amewatambua kwa majina na kumjeruhi kwa kumpiga nondo kichwani ,DMX alivamiwa usiku wa juzi eneo la Makorongoni katika Manispaa ya Iringa
 
Chanzo: www.francisgodwin.blogspot.com

DAR ES SALAAM

KUONA MECHI YA STARS NA DRC TSH 2,000


Kiingilio kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) itakayofanyika Februari 23 mwaka huu kitakuwa sh. 2,000 kwa viti vya kijani na bluu.
 
Mechi itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo viti hivyo vya kijani na bluu vinachukua watazamaji 36,693 ambayo ni karibu theluthi mbili ya viti vyote kwenye uwanja huo wa kisasa.
 
Viti vya rangi ya chungwa kiingilio ni sh. 5,000, VIP C itakuwa sh. 7,000 wakati VIP B tiketi zitauzwa kwa sh. 10,000. Kiingilio kwa viti vya VIP A kitakuwa sh. 15,000.
Kwa vile Februari 23 mwaka huu ni siku ya kazi ili kutoa fursa kwa washabiki wengi kushuhudia pambano hilo la kimataifa, mechi hiyo itaanza saa 11 kamili jioni.
 
Wakati Taifa Stars inayofundishwa na Jan Poulsen imeingia kambini leo na ikitarajiwa kuanza mazoezi jioni kwenye Uwanja wa Karume, DRC ambayo iko chini ya kocha Claude Le Roy inatarajia kutua nchini kesho.
 
Taifa Stars na DRC zinatumia mechi hiyo kunoa wachezaji wao kabla ya mechi zao za mchujo za Kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini. 
 
Katika raundi hiyo ya awali ambayo mechi zake zitachezwa Februari 29 mwaka huu, Stars itaanzia nyumbani dhidi ya Msumbiji wakati DRC inaanzia ugenini dhidi ya Seychelles.
 
Chanzo: francisgodwin.blogspot.com
 

IRINGA

INATISHA NI BAADA YA KUSHINDWA KUUA AJICHOMA KISU SHINGONI

Mwanamke ambae bado hajafahamika jina wala anakoishi katika mkoa wa Iringa akiwa hoi baada ya kujichoma kisu shingoni mwenyewe kwa kile kinachodaiwa kuwa ni baada ya mwenyeji wake kumkimbia na kujificha chooni kukwepa kuuwawa na mwanamke huyo asubuhi ya leo eneo la Frelimo mjini Iringa(picha zinatisha sana naomba radhi kwa usumbufu )
Hapa akikimbizwa hospitali ya mkoa na askari polisi waliofika kunusuru maisha yake

Chanzo: francisgodwin.blogspot.com

Sunday, February 19, 2012

KENYA

Wanaume wagoma kula majumbani mwao

 20 Februari, 2012 - Saa 05:55 GMT
Nderitu Njoka, mwenyekiti wa chama cha wanaume akimfariji baba aliyepigwa na mkewe

Waume nchini Kenya wanapanga kugomea vyakula vya mabibi zao kwa siku sita kutoka na kuongezeka kwa visa vya wanawake kuwapiga mabwana zao.
Badala yake wanaume watakuwa wakila mahotelini na magengeni

Mwenyekiti wa Chama cha maendeleo ya Kina baba Nderitu Njoka amesema mgomo huo wa siku sita una lengo la kuwashinikiza wanawake kukoma kuwanyanyasa na kuwapiga waume zao.

Kiongozi huyo Nderitu Njoka amesema kuanzia leo jumatatu ataanza kampeni ya kuwashawishi akinababa kula mahotelini badala ya majumbani mwao.

Mwenyekiti huyo wa maendeleo ya wauaume alikuwa akizungumza katika hospitali kuu ya mjini Nakuru huko Rift valley ambako alikuwa amekwenda kumliwaza baba mmoja ambaye amelezwa humo kutokana na kipigo alichopewa na mkewe.

Baba huyo akizungumza kwa uchungu hospitalini alisema mkewe alimuita nyumbani it akachukuwe pesa kabla ya kumfungia chumbani na kumtandika.

Kwa muujibu wa bwana Nderitu Njoka, mkoa wa kati nchini Kenya ndio unaongoza kwa idadi ya akina baba wanaopigwa na bibi zao.

Katika mkoa huo wa kati wanaume karibu nusu milioni wameripoti kutandikwa.
Chama hicho cha wanaume kimedai kuwa kuna wanaume ambao wanalazimishwa kufuo nguo za wake zao.
Wengine pia wamedai kunyimwa tendo la ngono na mabibi zao.

Jijini Nairobi wanaume ambao huona kivumbi kutoka kwa wake zao ni laki tatu.
Lakini baadhi ya akina mama kutoka mkoa huo wanasema akina baba ndio wa kulaumiwa kwa kushindwa na majukumu yao ya kifamila.

Wanasema waume wangi wamekuwa waume suruali tu.
Hata hivyo wengi wanasubiri kuona kama kweli mgomo huo utafaulu, na ni wanaume wangapi walio na pesa za kwenda kula hotelini badala ya kula majumbani mwao.

Chanzo: BBC Swahili

HUU NI UNYAMA WA KUTISHA IRINGA  

"KIJANA ACHOMA KISU UTUMBO WATOKA NJE"

mpenzi mdao wa mtandao huu kwanza naomba radhi kwa picha hizi za kusikitisha ila ndio hali halisi ya mambo inatisha sana Kijana kizito Kimeya (28) mkazi wa kijiji cha Mkoga kata ya Isakalilo Manispaa ya Iringa akiwa Hospitali ya mkoa wa Iringa kupatiwa matibabu baada ya kuchomwa kisu na utumbo wake kutoka nje
Miguu ikiwa imekatwa katwa mapanga na wauwaji hao ambao hawakufanikiwa kutimiza azmayao
hapa utombo ukiwa nje baada ya kuokolewa na afisa mtendaji wa kata hiyo ya Isakalilo Iringa mjini
Ni vigumu kuamini kama kweli kuna binadamu na wanywa damu ila kutokana na matukio kama hayo ndipo unaweza kuamini kuwa wapo binadamu na wanywa damu baada ya watu wanne ambao majina yao yametajwa na kijana huyo kudaiwa kumchoma visu kijana huyo pichani baada ya kumfuma akiiba mahindi ya mabichi maarufu kama Gobo katika shamba lao

Kijana huyo alichomwa kisu na kucharangwa mapanga na baada ya wahusika kutenda unyama huo walimchukua na kumweka katika mfuko wa sarufeti na kujaza mchanga na kisha kumtupa mtoni kabla ya na kusindwa katika maji kwa masaa zaidi ya matano na baadae maji kusaidia kuupasua mfuko huo na mchanga wote kumwagika na kijana huyo kujisaidia kujikokota hadi nje kavu na kukutwa porini siku ya pili yake majira ya saa 1 usiku na wasamaria wema.

Chanzo: http://www.francisgodwin.blogspot.com

Saturday, February 18, 2012

DAR ES SALAAM

YANGA YALAZIMISHWA KUONGEA KIARABU NA ZAMALEK UWANJA WA TAIFA

Wachezaji wa timu ya Yanga wakishangilia mbele ya mashabiki wao mara baada ya mchezaji wa timu hiyo Khamis Kiiza, kuifungia timu hiyo goli la kuongoza katika kipindi cha kwanza,Tayari mpira umekwisha na timu ya Zamalek imefanikiwa kusawazisha goli na kufanya matokeo kuwa 1-1 mpaka mwisho wa mchezo.Huu ni mchezo wa mashindano ya Klabu bingwa barani Africa yanayoandaliwa na shirikisho la vyama vya mpira wa miguu (CAF), timu hizo zitarudiana tena nchini Misri baada ya wiki mbili zijazo.
Mmoja wa wachezaji wa Yanga akipiga mpira kuelekea lango la Zamalek huku mlinda mlango wa timu hiyo akijaribu kuzuia ili mpira huo usilete madhara katika lango lake.
Mashabiki wa timu ya Yanga wakiwa wamevamia kweny jukwaa la Simba ambalo mashabiki wa Simba wanakaa.
Wachezaji wa Yanga na Zamalek wakisalimiana kabla ya kuanza kwa mchezo huokwenye uwanja wa Taifa.
Marefarii wa mchezo huo wakiziongoza timu kuingia uwanjani tayari kwa kuanza kwa mchezo huo.
 
Chanzo: Kapingaz blog

Zimbabwe yaondolewa vikwazo na EU

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe

Muungano wa Ulaya umewaondolea vikwazo baadhi ya maafisa wakuu wa serikali ya Zimbabwe, ingawa utaendelea kushikilia mali ya rais wa nchi hiyo Robert Mugabe pamoja na washirika wake wa karibu.
Kwa mujibu wa muungano huo, vikwazo vya usafiri dhidi ya mawaziri wawili viliondolewa ili kushinikiza serikali kuharakisha mchakato wa mageuzi.

Lakini msemaji wa chama cha rais Robert Mugabe,alipinga hatua hiyo akitaja vikwazo hivyo kama vinavyokiuka sheria, vyenye misingi ya ubaguzi wa rangi na vitakavyoathiri uchumi wa nchi.
Muungano huo pia uliondoa takriban kampuni ishirini za serikali kwenye orodha hiyo ambazo muungano huo ulidai kuwa zilisaidia kufadhili vurugu nchini Zimbabwe.

Ingawa Zimbabwe imepiga hatua katika mchakato wa kuunda katiba mpya, na kuimarisha uchumi, Muungano huo ungali na wasiwasi ikiwa ahadi zilizowekwa baada ya uchaguzi uliokumbwa na vurugu mwaka 2008, ikiwemo ahadi za kufanyia mabadiliko idara ya polisi hazijaweza kutimizwa.

DAR ES SALAAM

Yanga, Zamalek hapatoshi leo. 

Na:Sosthenes Nyoni na Calvin Kiwia 
MABINGWA wa soka nchini, Yanga leo watashuka dimbani wakiwa na deni la kucheza kufa na kupona ili kuepuka kuithibitisha kauli ya wapinzani wao Zamalek ya Misri kwamba, wamekuja nchini kuwafanya wao kuwa ngazi ya kutwaa ubingwa wa Vilabu Afrika.
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Kocha Msaidizi wa timu ya Zamalek ya Misri Osama Nabil (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,katikati ni msemaji wa TFF Boniface Wambura anayefuata ni Kocha Mkuu wa Yanga Kostadin Papic pamoja na Nahodha wa Yanga Shadrack Nsajigwa.Picha na Mpiga picha Wetu.
 
Mchezo huo ulioteka hisia za mashabiki wa soka nchini, unatarajia kuwa mkali ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia majira ya saa 10 jioni.

Jana katika mkutano na waandishi wa habari jijini, Kocha Msaidizi wa Zamalek, Ossama Nabil alisema wamekuja Tanzania siyo tu kuifunga Yanga, bali nia yao kubwa ni kutwaa ubingwa baada ya muda mrefu.

Nabil alisema ni muda mrefu sasa umepita bila timu yao kutwaa taji kubwa la soka Afrika, hivyo fursa ya pambano la leo dhidi ya Yanga ambalo wana hakika watashinda ni njia nzuri kuelekea kurejesha taji hilo.

"Tunaiheshimu Yanga kama klabu kubwa na yenye uzoefu kwenye michuano hii, lakini pamoja na hilo kwa upande wetu tunataka kulirudisha kombe la michuano hii katika mikono yetu baada ya kulikosa kwa muda mrefu," alisema kocha huyo msaidizi.

"Tumekuja hapa siyo tu kuifunga Yanga, lakini pia mechi ya hiyo ni fursa yetu nzuri ya safari ya kutwaa taji tulilolikosa kwa muda mrefu sasa," alisema Nabil kwa kujiamnia.

Nabil alisema kuwa kikosi chake kiko imara na chenye kila utayari wa ushindani dhidi ya Yanga. "Tumekuja tukiwa tumejiandaa vizuri, tumekuja kufurahia ushindi."

Kwa upande wa Kocha, Kostadin Papic ambaye mwanzoni alionyesha kukata tamaa ya kuzaimisha Zamalek nyumbani, jana alitoa kauli za kujivunia maandalizi aliyofanya kwenye kikosi chake.
"Nimemaliza jukumu la maandalizi kwa timu yangu, nimendaa kikosi cha ushindani kinachojiandaa kukabiliana vizuri na Zamalek," alisema Papic katika mkutano na waandishi wa habari.

Papic hakutaka kuibeza Zamalek kama alivyofanya mwenzake, lakini yeye anaamini anacheza na moja ya timu bora kabisa katika soka la Afrika.

"Kama kocha nimemaliza kazi yangu, ninaweza kusema tupo tayari kupambana na Zamalek katika pambano hili gumu. Hatuna la zaidi uwanjani zaidi ya ushindi," alisema Papic

Pamoja na maandalizi hayo, Papic atashusha kikosi kitakachokuwa na makali pungufu kutokana na baadhi nyota wake kuwa nje kutokana na kuwa majeruhi.

Ni wazi kipa namba moja, Yaw Berko hatakuwa uwanjani leo, sawa kama ilivyo kwa viungo Salum Telela, Godfrey Bonny, Nurdin Bakar na Rashid Gumbo.

Na badala yake, Yanga itawategemea zaidi washambuliaji wake Devis Mwape na Kenneth Asamoa kupeleka mashambulizi langoni mwa Zamalek wakipitishiwa mipira na kiungo Haruna Niyonzima.

Kwa upande wa kikosi cha mafarao, mshambuliaji zamani wa Wigan Athetic, Amri Zaki ndiye anayetarajia kuwa mwiba mkali kwa Yanga sambamba na Mcameroon Alex Mdomo na Razack Thomas ambaye ni raia wa Benin.

Wakati huo huo, nyota wa zamani wa Yanga, Athuman Chama 'Jogoo' amemtaka kocha wa timu hiyo, Mserbia Kostadin Papic kutumia mfumo wa 4-4-2 badala ya 4-3-3 kwenye pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek.

Beki huyo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars alisema: "Tangu Papic alivyotua nchini mwaka jana kukinoa kikosi cha Yanga amekuwa akitumia mfumo wa 4-3-3," alisema Chama.
Amekuwa akiwachezesha Mwape, Asamoah na Kiiza nafasi ya ushambuliaji wakati Kijiko, Seme na Niyonzima wakicheza katikati ya kiwanja.

"Sioni kama mfumo huo unatoa matumaini chanya yakuishinda Zamalek kwa leo, ambao wana uwezo mkubwa wakumiliki mpira na kupiga pasi kutoka njuma hadi mbele kushambuliaji," alisema Chama.

Alisema anafikiri mfumo wa 4-4-2 ndio utatoa nafasi kubwa kwa Yanga kuweza kuwadhibiti vilivyo Waarabu hao.

"Unavyotumia mfumo wa 4-4-2 ina maana utakuwa na wachezaji wanne katikati ya kiwanja ambao watakuwa na kazi ya kuzuia na pia kushambulia kwa wakati mmoja," aliongeza Chama.
"Lakini unavyotumia 4-3-3 unapunguza mtu mmoja katikati ya uwanja na kumpeleka mbele kushambulia, zitaki kuamini kwamba Kiiza ana uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji," alisema.

Alishauri kocha huyo kutumia mfumo wa 4-4-2 kwa lengo la kuwadhitibiti Zamalek na kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye pambano hilo la awali na kujiweka katika mazingira mazuri kusonga mbele ya michuano hiyo. 

Chanzo: Mwananchi Communications Ltd