Utafiti mpya unasema utapiamlo ni kiini kinachosababisha vifo kwa watoto wapatao milioni 2.6 kila mwaka.

Ripoti kutoka kundi moja la kimatiafa la kutoa misaada  la Save the Children, inasema licha ya juhudi za ulimwengu kumaliza njaa utapiamlo unabaki kuwa tatizo kubwa lililopuuzwa ambalo linaathiri robo ya watoto ulimwenguni.

Utafiti uliofanywa mwezi Disemba na Januari unasema kwamba watoto 300 wanakufa kila saa kwa sababu ya utapiamlo.

Kundi linasema kuongezeka kwa bei ya chakula kumelazimisha watoto katika nchi nyingi kuacha shule ili kusaidia familia zao kupata fedha.

Katika kesi nyingi, ripoti ilisema utapiamlo haukuwa matokeo pekee ya kutokuwa na chakula cha kutosha, lakini kwa sababu familia haziwezi kumudu kupata chakula bora.

Save the Children linamsihi Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kufanya mkutano juu ya njaa duniani pembeni ya michezo ya Olympic mwaka 2012 itakayofanyika huko London baadae mwaka huu.

Shirika lilisema asilimia 90 ya watoto wengi wasiojiweza duniani wangeweza kulindwa kutopata utapiamlo kwa kiwango  kidogo cha dola bilioni 10 kwa mwaka.