

Na Rhobi Chacha
HABARI zilizotua juu ya dawati la Risasi Jumatano wiki hii zinadai kuwa msako mkali unaendelea mkoani Mtwara, waganga wa kienyeji wanaingia nyumba hadi nyumba kunasa wachawi, aya zinazofuata zinaachia kila kitu.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, waganga hao walifika hadi kwenye kijiji alichozaliwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Hawa Abdurahman Ghasia.
NI NYUMBA KWA NYUMBA
Inadaiwa waganga hao wamo mkoani humo kwa operesheni maalum kufuatia agizo ambalo mpaka sasa haijajulikana nani alilitoa.
Habari zaidi zinasema kuwa zoezi hilo kwa sasa limeshamiri na kuingia kata kwa kata na nyumba hadi nyumba.
Chanzo kikaendelea kudai kuwa baada ya amri ya kuwepo kwa zoezi hilo, nyumba kadhaa zimekumbwa na kashikashi hiyo ya kushangaza.
Kijiji alichozaliwa Waziri Ghasia ni Naumbu, Kata ya Mikindani, Mtwara Vijijini ambapo habari zinadai karibu wakazi wake wote ni ndugu na wanaishi kwa umoja.
Chanzo: “Lakini ndani ya baadhi ya nyumba walikuta vitu vya ajabu, nyingine hawakukuta vitu.” Kikaendelea kudai: “Katika safari hiyo, wakafika kwenye nyumba ya bibi mmoja (jina halikupatikana mara moja), humo inadaiwa walinasa vitu lakini haikujulikana kama ni vya uchawi au la!”
WAANDISHI WAMBANA MBUNGE
Naye Ripota Wetu wa Mtwara, Sijawa Omary anasema kuwa baada ya waganga kupekua nyumba mbalimbali za eneo hilo, waandishi wa habari mkoani humo walimwita Waziri Ghasia ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini na kuzungumza naye wakimtaka aeleze alichonacho kuhusu zoezi la ‘wasakaji’ hao.
Waziri huyo, pamoja na mambo mengine hakuonesha uhalali wa kuwepo kwa operesheni hiyo na hivyo kutotolea ufafanuzi wa kutosha.
VIGOGO WAUMBUKA
Naye mwenyekiti wa kijiji kimoja mkoani humo ambaye aliomba majina yake na ya kijiji yasitiriwe, alisema zoezi hilo limeumbua watu mkoani Mtwara, lakini pia amejifunza kuwa, wapo binadamu ambao kwa macho ni wazuri, lakini usiku wana mambo yao ya hatari.
“Zoezi linaendelea lakini ukweli ni kwamba kuna vigogo wameumbuka. Kumbe unaweza kumwona mtu mchana ukaamini ni mwema, usiku ni adui, hii ni hatari,” alisema mwenyekiti huyo.
WAFANYABIASHARA WAFURAHIA
Aidha, habari zaidi zinasema kuwa, uchawi unaovuma zaidi mkoani humo kwa sasa unaitwa Mang’opo ambapo wafanyabiashara wanaibiwa fedha zao bila kujijua.
“Huku Mtwara unaweza ukafanya biashara yako kuanzia Januari mpaka Desemba usione fedha iliyoingia, wewe kila siku ni kutoa kwa ajili ya kuendesha biashara lakini faida haionekani.
“Ukiona hivyo ujue wapo wataalamu tayari wanakula fedha yako. Wapo wale ambao wanajifanya ombaomba, ole wako umpe fedha na aone kwenye pochi yako kuna kiasi gani, utakuja kushangaa hakuna fedha.
“Ama kuna ile ya kutoa fedha dukani ambayo itahitaji chenji, ole wako ile chenji uichanganye na fedha zako nyingine katika pochi, utalia,” alisema mwanakijiji mmoja huku akikataa kutaja jina lake.
Hata hivyo, habari za uhakika zinadai kuwa, baadhi ya wachawi wametoa Mang’opo yao ndani ya nyumba na kwenda kuchimbia chini ya ardhi wakisubiri zoezi hilo lipite.
Risasi Jumatano juzi Jumatatu lilimtafuta Waziri Ghasia ili azungumzie sakata hilo na alipopatikana alisema: “Ni kweli waganga hao walifika katika kijiji chetu na kufanya upekuzi kuhusiana na masuala ya ushirikina.
“Walifanya hivyo katika nyumba mbalimbali lakini kwenye nyumba yangu na ya wazazi wangu hawakupekua.”
KAMANDA WA MKOA AZUNGUMZA
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nkuzi alipoulizwa na Risasi Jumatano kuhusu sakata hilo alikiri kutokea.
“Ni kweli kumekuwa na hali hiyo, watu wanaojiita waganga wamekuwa wakiingia nyumba hadi nyumba na kudai wanatoa vitu vya uganga, lakini serikali imeanza kuwakamata na baadhi yao wamefikishwa mahakamani,” alisema Afande Nkuzi.
Habari hii ni kwa hisani ya Global Publishers
No comments:
Post a Comment